Timu ya Wataalamu kutoka Ofisi ya Rais (TAMISEMI) pamoja na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi Public Private Partnership Center (PPPC), kilichopo chini ya Wizara ya Fedha, wamefanya kikao kazi na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Ndg. Abushiri Mbwana, kwa lengo la kutoa elimu na kufanya majadiliano juu ya fursa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia ubia kati ya Halmashauri na Sekta Binafsi.
Kikao hicho kimefanyika tarehe 14 Aprili 2025 katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, ambapo wadau hao walijadili maeneo muhimu ya uwekezaji yanayoweza kufanikishwa kupitia mfumo wa PPP (Public Private Partnership), ikiwa ni njia mbadala ya kuongeza ufanisi na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika ngazi ya Serikali za mitaa.
Katika kikao hicho, elimu kuhusu miongozo ya PPP, vigezo vya uteuzi wa miradi, taratibu za kisheria na faida kwa Halmashauri zilitolewa, huku pande zote zikiwa na nafasi ya kutoa maoni na mapendekezo ya miradi yenye tija kwa jamii ya Kilwa.
Akizungumza katika kikao hicho, Ndg. Abushiri Mbwana ameeleza kuwa Halmashauri ya Kilwa iko tayari kushirikiana na sekta binafsi katika kuendeleza miradi yenye tija kwa Wananchi, kwa kuzingatia Misingi ya uwazi, tija na uendelevu.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa