Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa imefanya kikao maalum na wadau kutoka Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika kutekeleza shughuli za kijamii na kuisaidia jamii Wilayani Kilwa.
Kikao hicho, kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Kilwa tarehe 01 Julai, 2025, kimewaleta pamoja wawakilishi kutoka mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali ambapo washiriki walipata nafasi ya kujadili namna bora ya kuimarisha mahusiano kati yao na Serikali.
Akifunga kikao hicho, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilwa, Ndg. Yusuf Mwinyi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kilwa amewapongeza viongozi na wawakilishi wa mashirika hayo kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuunga mkono juhudi za Serikali, hususani katika kusaidia jamii zenye mahitaji maalum kama waathirika wa mafuriko na watu wanaoishi katika mazingira magumu.
"Tunatambua na kuthamini mchango wenu mkubwa kwa jamii. Ushirikiano kati ya mashirika yasiyo ya kiserikali ni muhimu sana katika kuleta maendeleo " amesema Ndg. Mwinyi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Ndg.Grace Mwambe, ameeleza kuwa lengo kuu la jukwaa hilo ni kuimarisha uhusiano na mshikamano kati ya Serikali na mashirika hayo, pia kuwakumbusha kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya serikali katika utekelezaji wa shughuli za kuisaidia jamii ikiwemo kulipa ada na tozo kwa wakati ili kuwezesha Serikali kutoa huduma bora kwa wananchi.
Aidha, ametoa wito kwa mashirika hayo kuendelea kusaidia wanafunzi wanaotoka katika familia zenye hali duni, ili kuwawezesha kuendeleza masomo yao na kutimiza ndoto zao, jambo ambalo litaleta tija kwa familia zao na taifa kwa ujumla.
Jukwaa hilo litaenda kuwa na tija kwa pande zote mbili kwa kuendeleza ushirikiano wa maendeleo endelevu katika Wilaya ya Kilwa pia ni sehemu ya juhudi za Halmashauri kuhakikisha maendeleo jumuishi kupitia ushirikiano thabiti kati ya Serikali na wadau wa maendeleo
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa