Katika kuhitimisha mafunzo ya siku tatu (3) ya ukusanyaji wa takwimu za rasilimali za bahari kidigitali (Kobo Collect). Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Ndg. Hemed S. Magaro, amekabidhi simu janja 33 zenye thamani ya Tsh 8,910,000/= kwa Vikundi 11 vya usimamizi wa fukwe (BMU) Kilwa Kusini, zilizotolewa na Shirika la Sea Sense kupitia uwezeshaji kutoka Shirika la Blue Venture, ili zitumike katika ukusanyaji wa takwimu kwa njia ya kidigitali.
Pia katika hafla hiyo Ndg. Magaro amekabidhi vifaa vyenye thamani ya Tsh 6,000,000/= vitakavyo tumiwa na BMU katika upumzishaji wa miamba ya uvuvi ambavyo ni mafuta lita 600, kamba mita 90 kumi (10), maboya makubwa 15, mizani 15, chachacha 15, snuka (snooker) 10, mask 10, Pezi bandia (flipper) 10, mifuko ya saruji 5, nondo 5, tochi 10 na fedha taslimu shilingi 150,000.
Zoezi la ugawaji wa vifaa hivyo limefanyika tarehe 15 Mei 2025 katika Ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Kilwa,
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Ndg. Magaro ameeleza kuwa mafunzo haya na vifaa vilivyotolewa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa takwimu na kuongeza utunzaji wa Ikolojia ya bahari na usimamizi wa rasilimali za uvuvi. Aidha, ameagiza Kitengo cha Uvuvi, BMU, pamoja na serikali za vijiji kuhakikisha kuwa vifaa hivyo vinatunzwa ipasavyo na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Mtakapokusanya takwimu sahihi kwa wakati, mtaiwezesha serikali kupanga mipango bora ya maendeleo kwa sekta ya uvuvi,” amesema Ndg. Magaro.
Mafunzo haya yametolewa na Shirika la Sea Sense kwa kushirikiana na Serikali ya Wilaya ya Kilwa, ikiwa ni juhudi za pamoja za kuinua sekta ya uvuvi na kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa