Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Ndg. Hemed Magaro amekabidhi pikipiki aina ya Kinglion XL 150 kwa Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za uhifadhi na utunzaji wa mazingira.
Tukio hilo limefanyika tarehe 18 Septemba 2025 katika Ofisi za Halmashauri ya Kilwa, ambapo pikipiki hiyo muhimu itarahisisha kazi za kudhibiti uharibifu wa mazingira, usimamizi wa wanyama pori, pamoja na kulinda rasilimali za misitu na maliasili nyingine katika maeneo mbalimbali ya wilaya.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Ndg. Magaro alisema kuwa halmashauri itaendelea kuweka kipaumbele katika kulinda rasilimali za asili na kuhamasisha jamii kushirikiana na Serikali katika kuimarisha uhifadhi, kupanda miti, na kuepuka shughuli zinazohatarisha mazingira ili kulinda vizazi vya sasa na vijavyo.
Hatua hii ni sehemu ya juhudi endelevu za Halmashauri kuboresha ulinzi wa rasilimali asilia, kuimarisha uhifadhi wa mazingira, na kuhakikisha jamii inanufaika na mazingira salama na endelevu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira Ndg. Abushiri Mbwana ameishukuru Halmashauri kwa msaada huo na kuahidi kuutumia ipasavyo ili kuhakikisha malengo ya uhifadhi yanafikiwa kikamilifu, huku akihimiza wananchi kushirikiana na Serikali katika kulinda rasilimali za asili.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa