Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Ndg. Hemed Magaro, amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika sekta za Afya na Elimu, ili kuhakikisha inatekelezwa kwa viwango vinavyokubalika na kukamilika kwa wakati.
Ziara hiyo imefanyika tarehe 12 Agosti 2025 katika Kata za Kikole, Njinjo na Miguruwe, ikihusisha timu ya wataalamu kutoka idara mbalimbali za Halmashauri kwa ajili ya kufanya tathmini ya maendeleo ya miradi inayotekelezwa kupitia vyanzo mbalimbali vya fedha.
Ametembelea Shule ya Msingi Mbate kukagua ujenzi wa madarasa mawili (Sh. milioni 48) na umaliziaji wa nyumba ya mwalimu (Sh. milioni 19). Vilevile, amekagua mradi wa mabweni ya wanafunzi katika Shule ya Sekondari Njinjo (Sh. milioni 185) unaofadhiliwa na Shirika la ActionAid, pamoja na ujenzi wa vyoo katika Shule ya Sekondari Miguruwe (Sh. milioni 8.5) na choo cha nyumba ya mwalimu Shule ya Msingi Zingakibao (Sh. milioni 2.98) kupitia Mfuko wa Jimbo.
Katika sekta ya afya, ametembelea ujenzi wa Zahanati ya Njinjo (Sh. milioni 249.12) unaofadhiliwa na Serikali Kuu, Zahanati ya Miguruwe (Sh. milioni 130) kupitia mapato ya ndani, na nyumba ya Mganga (Sh. milioni 50) kwa ushirikiano wa Serikali na wananchi. Pia, amekagua umaliziaji wa Jengo la Upasuaji na Wodi ya Wazazi katika Zahanati ya Zingakibao (Sh. milioni 450) kupitia mapato ya ndani.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Ndg. Magaro amesema "Tunataka miradi hii itekelezwe kwa viwango vya kitaalamu. Wananchi wasubiri huduma bora, si hadithi."
Ameongeza kuwa amewasihi wenye miradi ya mashirika yasiyo ya kiserikali kuhakikisha inasimamiwa kwa makini na kwa weredi sawa na miradi mingine ya Serikali.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa