Kilwa,
Mkuu wa wilaya ya kilwa Mheshimiwa Christopher Ngubiagai amegawa bidhaa zenye thamani ya zaidi ya Milioni Arobaini na Tano kwa Shule za Sekondari, Msingi, Taasisi za kiserikali, Vituo vya kulelea watoto Yatima na wenye Mahitaji maalumu.
Bidhaa hizo ni viroba Mia mbili na kumi na Sita vya sukari pamoja na Madumu Mia Tatu Arobaini na Nane ya Mafuta ya kupikia ambazo ni miongoni mwa Viroba Mia Nne na Hamsini na Dumu Elfu moja Mia Tatu arobaini na tisa yaliyokamatwa kwa kosa la kuingizwa Wilayani Kilwa kinyume na utaratibu kati ya mwezi Februari na Juni.
Akizungumza wakati wa ugawaji wa Bidhaa hizo Mheshimiwa Ngubiagai amesema Serikali ya awamu ya Tano ina nia njema ya kuwasaidia Wafanyabiashara ili waweze kunufaika na wanachokifanya na kuwataka kuheshimu na kufuata utaratibu ambao umewekwa na Serikali.
Ngubiagai amesema Kamati ya ulinzi na Serikali kwa ujumla ipo Macho kuhakikisha inawakamata na kuwachukuliwa hatua za kisheria. wale wote ambao wanaingiza Bidhaa kinyemela kupitia bandari Bubu.
“Wafanyabiashara tushirikiane kulipa kodi na tozo mbalimbali ambazo zipo kisheria ili tuweze kupata mapato ambayo yatasaidia kuimarisha huduma mbalimbali za kijamii na kukuza viwanda vyetu
Serikali ipo Macho saa Ishirini na Nne kuhakikisha inawakamata wale wote ambao wanakwepa kulipa Kodi na Tozo mbalimbali na kuingiza Bidhaa kinyemela kupitia bandari Bubu, wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria” alisema Ngubiagai
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Christopher Ngubiagai akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kukabidhi Bidhaa mbalimbali kwa Shule, taasisi za serikali na wenye mahitaji maalumu (Picha: Ally Ruambo).
Pia ameitaka jamii kushirikiana na serikali kwa kuwafichua Wafanyabiashara ambao wanaingiza Bidhaa zao kupitia bandari zisizo rasmi na kukwepa kulipa kodi.
Aidha amewata Walimu na Wasimamizi wa Makambi ya Wanafunzi wanaojiandaa na Mitihani yao mwisho kutumia Sukari na Mafuta waliyopatiwa kwa uangalifu na kwa manufaa ya wanafunzi.
“Hivi vitu tulivyotoa sio kwa niaba yenu walimu ni kwa ajili ya Wanafunzi, ni marufuku kuuza au kwenda kutumia nyumbani kwako, Tumetoa kwa ajili ya vijana wetu ambao wako Mashuleni na wale ambao wapo Makambini wakijiandaa na Mitihani ya mwisho
Wapelekeeni wakale washibe ili wapate nguvu ya Kusoma na hatimaye waweze kufanya vizuri katika Mitihani yao na Malengo yetu ya kupandisha Elimu Wilaya ya Kilwa yatimie, na Kikosi kazi kitakuja kutembela na kukagua kila Shule na Kambi kuona Maendeleo na Changamoto ambazo zipo huko” alihitimisha Ngubiagai.
Walimu na Viongozi kutoka Taasisi mbalimbali wakibeba Viroba vya Sukari baada ya kukabidhiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mheshimiwa Christopher Ngubiagai (Picha: Ally Ruambo)
Jumla ya Madumu Elfu Moja na Moja na viroba Mia mbili na Thelathini na Nne vilivyobaki katika mgawo huwo vinatarajiwa kugawanywa katika Wilaya Nne ambazo zinaunda Mkoa wa Lindi.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa