Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi,Christopher Ngubiagai amewaonya viongozi na watendaji wa vijiji wilayani humu kuwa makini na mikataba ya ardhi wanayofanya na wawekezaji.
Ngubiagai alitoa wito jana alipozungumza na wananchi wa kijiji cha Mtukwao,kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho kilichopo katika kata na tarafa ya Miteja.
Alisema serikali imevipa vijiji mamlaka kamili kuhusu ardhi kupitia sheria namba 5 ya ardhi ya mwaka 1999.Hata hivyo wananchi wasitumie uwezo huo vibaya na kusababishia vijiji kushindwa kunufaika na raslimali na maliasili hiyo iliyopo kwenye vijiji.Hali ambayo inasababishwa na viongozi wachache wanaoshirikiana na wawekezaji kuwadhulumu wananchi.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona vijiji na hata wilaya hiyo ikiwa taabani kiuchumi wakati vinazungukwa na maliasili nyingi.Huku mikataba inayofanywa na baadhi ya wawekezaji ikiwa haina tija kwa halmashauri wala wilaya hii.
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Christopher Ngubiagai akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mtukwao katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho kilichopo katika kata na tarafa ya Miteja.
Alisema baadhi ya viongozi na watendaji wameingia mikataba na wawekezaji wababaishaji wasio na uwezo ambao wameshindwa kuendeleza maeneo waliyopewa.Huku vijiji vikiwa havipati chochote.
Aliwataka viongozi wa vijiji ambavyo wawekezaji wameshindwa kuendeleza maeneo waliyowapa,wahakikishe wanawaita na kuwapa muda wa kuyaendeleza.Iwapo watashindwa kuendeleza wanyang'anywe ili wapewe wawekezaji wenye uwezo.
"Nijambo la aibu kuona vijiji vimezungukwa na maliasili nyingi,lakini havina hata ofisi.Ukiangalia mikataba iliyofanyika haina tija," alisema Ngubiagai.
Aliwataka viongozi kuwa makini na mikataba ili wawapunguzie mzigo wa shida wananchi wao ambao wanahitaji maendeleo na kufaidika na maliasili zinazowazunguka.Ambazo ni tunu kutoka kwa Mungu.
Wananchi wa kijiji cha Mtukwao wakiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho kilichopo katika kata na tarafa ya Miteja.
Mbali na hayo Mkuu huyo wa Wilaya ya Kilwa aliwapongeza wananchi wa kijiji hicho kwa ushirikano wanaotoa kwa walimu na kamati ya shule.Ushirikaiano uliosababisha kuwa na kiwango cha 80% ya ufaulu.
Ngubiagai pia aliwapongeza wazazi na walezi wawanafunzi wanaosoma kwenye shule ya kijiji hicho kwa kuthibiti tatizo la mimba kwa wanafunzi wanaosoma kwenye shule hiyo.Huku akiweka wazi katika ziara atazofanya katika maeneo mengine atawahamasisha viongozi na wananchi wake kuiga yanayofanywa na wananchi na viongozi wa kijiji hicho.
Ngubiagai kwenye mkutano huo alihaidi kuchangia mifuko 20 ya saruji.Ikiwa ni mchango wake kwenye ujenzi wa ofisi ya serikali ya kijiji hicho cha Mtukwao.
Credit : Ahmad Mmow,Kilwa.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa