Kamati ya Afya ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa (CHMT) imetoa mafunzo maalum kwa wataalamu wa afya, viongozi wa dini, na wazee maarufu kuhusu umuhimu wa utoaji wa chanjo ya pili ya sindano ya polio. Mafunzo hayo yametolewa Tarehe 28 Aprili 2025 katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kampeni ya chanjo itakayofanyika Tarehe 1 Mei 2025 katika vituo vya afya mbalimbali wilayani humo.
Lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wadau hao ili wawe mabalozi wa kuelimisha jamii kuhusu chanjo hiyo muhimu, hasa kwa wazazi wenye watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mratibu wa Chanjo wa Wilaya ya Kilwa, Bi. Vickness Lutema, amesema kuwa chanjo hiyo ya pili ya sindano ya polio ni nyongeza muhimu katika kuongeza kinga dhidi ya ugonjwa huo.
“Chanjo hii inafanya kazi kwa ufanisi sawa na ile ya awali, lakini imeongezwa ili kuimarisha zaidi kinga ya mwili kwa watoto,” alisema Bi.Lutema
Bi. Lutema aliongeza kuwa kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa polio katika baadhi ya nchi jirani, Serikali ya Tanzania imechukua tahadhari za haraka kwa kuanzisha chanjo ya pili ili kuwalinda watoto wadogo ambao kinga zao za mwili bado ni dhaifu.
Aidha, alisisitiza kuwa chanjo hiyo ni salama na haina madhara kwa afya ya binadamu, na kuwataka wajumbe wote kuendelea kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika zoezi la chanjo hiyo.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa