Kilwa,
Mfuko wa Afya ya jamii umeboresha huduma zake ikiwemo kuondoa ukomo wa kutoa huduma ya matibabu kwa mwanachama kutoka ngazi ya Halmashauri mpaka ngazi ya mkoa.
Hayo yamebainishwa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko wa Afya ya jamii kutoka mfuko wa taifa wa bima ya afya makao makuu Ndg. Slivery Mgonza katika ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa vituo vya kutolea huduma ya Afya yaliyafanyika katika ukumbi wa chuo cha maendeleo Mjini Kilwa Masoko.
Mgonza amesema kabla ya maboresho mfuko ulikua na changamoto mbalimbali ikiwemo ukomo wa wanachama kupata matibabu katika vituo vya kutolea huduma ambayo kwa sasa imeondolewa kwa kufanyiwa maboresho.
“Kabla ya maboresho mwanachama alikua anatibiwa pale alipochangia na kwenye baadhi ya halmashauri alikua anaweza kwenda hadi hospitali ya wilaya lakini alikua hawezi kutoka nje ya Halmashauri, lakini pia hata huduma alizokua anapta zilikua zimefinywa kwa sababu alikua haewezi kulazwa au kufanyiwa upasuaji lakini kwa sasa tumefanya maboresho mwanachama atafaidika na mafao mengine zaidi na ataweza kutibiwa mpaka Hospitali ya rufaa ya mkoa”. Alisema Mgonza
Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko wa Afya ya jamii kutoka mfuko wa taifa wa bima ya afya makao makuu Ndg. Slivery Mgonza akizungumza na washiriki (awapo katika picha) katika ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa vituo vya kutolea huduma ya Afya yaliyafanyika katika ukumbi wa chuo cha maendeleo Mjini Kilwa Masoko. ( Picha na Ally Ruambo)
Amesema sanjari na mfuko wa Afya ya jamii kufanya maboresho katika kutoa huduma pia umefanya maboresho katika Nyanja ya usimamizi ambapo usimamizi umetolewa kutoka ngazi ya wilaya mpaka mkoani na Katibu tawala wa mkoa husika ndio atakua msimamizi wa utoaji huduma.
Kwa upande wake Meneja wa Mfuko wa Afya ya jamii wilaya ya Kilwa Bw. Fred Mpondachuma amewataka wananchi ambao hawajajiunga na mfuko wa afya ya jamii wajiunge sasa ili waweze kunufaika na huduma na kwa wale ambao ni wanachama wa mfuko wa afya ya jamii kuendelea kufurahia huduma za mfuko wa afya ya jamii na kujisajiri tena upya kwa gharama ya shilingi 30000 baada ya mkataba wao wa sasa kufikia mwisho.
Mmoja wa wakufunzi katika mafunzo kwa vituo vya kutolea huduma ya Afya Bi. Zabibu Uledi akielekeza jambo kwa washiriki wa mafunzo ya siku tatu kwa vituo vya kutolea huduma ya Afya yaliyafanyika katika ukumbi wa chuo cha maendeleo Mjini Kilwa Masoko. ( Picha na Ally Ruambo)
Awali akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya kilwa Bw. Zablon Bugingo amewataka wajumbe wa kamati na watendaji kushirikiana kwa pamoja katika kutekeleza majukumu yao ili kuleta matokeo chanya ambayo yatasaidia kusukuma gurudumu la maendeleo.
Aidha amewataka watumishi kuandaa kwa usahihi ripoti za kila mwezi na kuziwasilisha sehemu husika katika muda sahihi ili ziweze kufanyiwa kazi katika muda sahihi.
Mafunzo kwa vituo vya kutolea huduma ya Afya yamejumuisha watu mbalimbali ikiwemo wauguzi, waganga wafawidhi kutoka Hospitali na vituo vya afya mbalimbali, mwenyeviti na wajumbe wa kamati za afya za vijiji, afisa mifumo na wengineo.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya siku tatu kwa vituo vya kutolea huduma ya Afya yaliyafanyika katika ukumbi wa chuo cha maendeleo Mjini Kilwa Masoko. ( Picha na Ally Ruambo)
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa