Katika harakati za kutokomeza Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa Wilayani Kilwa, Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kupitia Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imeendelea na zoezi la utoaji wa Chanjo ya Kichaa cha Mbwa kwa lengo la Kudhibiti Ugonjwa huo Wilayani Kilwa ambapo hadi kufikia tarehe 14 Mei 2025, jumla ya Mbwa 1,524 na Paka 272 wamechanjwa dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa (rabies) katika Wilaya ya Kilwa,
Kati ya Mbwa 1,524 na Paka 272 Waliochanjwa, Mbwa 1,072 na Paka 206 Wamechanjwa kwa kutumia Chanjo binafsi kwa kutumia Maafisa mifugo walioko kwenye kata na vijiji mbalimbali na Mbwa 452 na Paka 66 wakichanjwa kwa kutumia chanjo zilizotolewa na Halmashauri na kusambazwa katika maeneo mbalimbali kipaumbele kikiwa ni maeneo yaliyoripoti milipuko ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa kwa wingi.
Huduma hii ya Chanjo inaendelea kutolewa na Maafisa Mifugo wa Kata katika Kata 16 amabazo ni Njinjo, Miguruwe, Kandawale, Likawage, Nanjirinji, Kiranjeranje, Mitole, Kikole, Masoko, Mandawa, Miteja, Somanga, Tingi, Namayuni, Mingumbi na Kivinje, Gharama ya Chanjo ni Tsh. 2,000/= kwa dozi ya mbwa mmoja.
Aidha, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Ndg. Shija Lyella amesema “Awali Halmashauri iliandaa Chanjo 1,000 kwa ajili ya zoezi hili ambazo zinaendelea kutolewa katika Kata 16 lakini pia Tunatarajia kuongeza chanjo nyingine 1,000 ili kukamilisha mahitaji ya Chanjo ya Kichaa cha Mbwa katika Wilaya yetu hivyo ni matarajio yetu kwamba tutaweza kuzifikia kata 7 zilizobakia".
Kwa upande wake Daktari wa Wanyama Wilaya ya Kilwa, Dkt. Ladslaus Massawe ameeleza kuwa kwa sasa kunatolewa huduma ya bure ya kutoa vizazi kwa mbwa jike (spaying) pamoja na kuhasi mbwa dume (neutering) il kupunguza uzalishaji holela wa mbwa na paka, na hivyo kudhibiti ongezeko la wanyama wasio na wamiliki katika jamii, ambao mara nyingi huwa chanzo cha kusambaza magonjwa kama kichaa cha mbwa.
Mwisho Dkt. Massawe ametoa wito kwa Wafugaji na wananchi wote kushiriki kikamilifu katika zoezi hili la chanjo na huduma za afya ya wanyama ili kulinda afya ya binadamu na wanyama kwa pamoja.
WAANDISHI WASAIDIZI NA WAENDESHA VIFAA VYA BAYOMETRIKI KATIKA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA AWAMU YA PILI WAAPISHWA KILWA
Afisa Mwandikishaji Wilaya ya Kilwa, Ndg.Msena Bina, Tarehe 14 Mei 2025 amewaapisha Waandishi wasaidizi wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wa Awamu ya pili ambapo zoezi hilo limefanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Kilwa.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo Ndg. Bina amewataka waandishi hao kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, huku akisisitiza umuhimu wa kutunza siri za kazi pamoja na vifaa vya kazi watakavyotumia wakati wa zoezi hilo muhimu la kitaifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Ndg Hemed Magaro ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mafunzo hayo, amesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa jamii katika uandikishaji,huku akitoa maagizo kwa waandishi ngazi ya kata kuhakikisha wanatumia makundi manne ambayo ni shule, viongozi wa dini, Wenyeviti wa Vitongoji na Viongozi wa Vyama vya Siasa ili kuweza kusaidia taarifa hiyo kufika kwa haraka wananchi.
“Ni muhimu taarifa kuhusu uandikishaji ziwafikie wananchi wote kwa haraka na kwa ufanisi. zoezi hili ni la kitaifa na kila mmoja anapaswa kushiriki kikamilifu” amesema Ndg. Magaro
Aidha, baada ya zoezi la kuapishwa, waandishi wasaidizi hao wanatarajiwa kupatiwa mafunzo ya siku moja kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya uandikishaji, ikiwemo namna ya kutumia Mfumo wa Usajili wa Wapiga Kura (VRS) ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi.
Zoezi hilo litafanyika kwa siku 7 kuanzia tarehe 16 Mei 2025 hadi tarehe 22 Mei 2025 Vituo vya kuandikishia wapiga kura vimepangwa katika kila Kata na vitafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa