Katika kuhitimisha ziara ya mafunzo ya ukusanyaji wa mapato na uhifadhi wa mazingira ya bahari mkoani Tanga, wanachama wa Vikundi vya Usimamizi wa Rasilimali za Bahari (BMU) kutoka Wilaya ya Kilwa wamepata elimu muhimu kuhusu Mfuko wa Kuhifadhi Bahari (MKUBA) kupitia semina iliyofanyika katika kijiji cha Kigombe, Wilaya ya Muheza tarehe 25 Juni, 2025.
Akizungumza wakati wa semina hiyo, Bi. Mwanahamisi Said Omary ambaye ni mwezeshaji wa masuala ya MKUBA, alieleza kuwa mfuko huo ni nyenzo muhimu katika kuwawezesha wavuvi kiuchumi kupitia mikopo isiyo na riba, elimu ya fedha, pamoja na kuwajengea uwezo wa kuanzisha biashara mbadala wakati wa kipindi cha ufungaji wa miamba.
“Mfuko huu unamwezesha mvuvi kukopa bila riba, na kupata elimu ya fedha na ujasiriamali ili kuendeleza maisha yao hata nje ya shughuli za bahari,” amesema Bi. Mwanahamisi.
Pamoja na elimu ya kifedha, wanachama wa BMU Kilwa walipata nafasi ya kujifunza kwa kina kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira ya bahari kutoka kwa Mhifadhi Mfawidhi wa Hifadhi ya Bahari ya Silikanti – Tanga (Marine Parks and Reserves - Tanga) Bi.Magreth Mchome ambaye aliwaeleza mbinu na mikakati ya kudhibiti uharibifu wa mazingira ya baharini kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Aidha Bi. Magreth alitoa wito kwa BMU za Kilwa kuchukua hatua madhubuti katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za bahari. Tunatoa wito kwa wanachama wote wa BMU kuanzisha na kuimarisha mifuko ya hifadhi kama MKUBA, ili kujenga uchumi imara kwa jamii zao, na wakati huo huo, kuwa walinzi wa mazingira ya bahari kwa maendeleo endelevu.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa