Baraza la Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wake Mhe. Rajab Msaka, wameridhia na kupitisha Mapendekezo ya kugawa Majimbo ya Uchaguzi ya Kilwa Kusini na Kilwa Kaskazini kwa lengo la Kuanzisha Jimbo Jipya la Kilwa Mashariki.
Hayo ni matokeo ya Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani uliolenga kujadili taarifa ya Mapendekezo ya Kugawa Majimbo ya Uchaguzi ya Kilwa Kusini na Kilwa Kaskazini ili Kuanzisha Jimbo Jipya la Kilwa Mashariki uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Kilwa Tarehe 10/03/2025.
Majimbo hayo matatu yamependekezwa kuundwa na Kata zifuatazo, Jimbo la Kilwa Kaskazini litakuwa na Kata ya Kipatimu, Kandawale, Chumo, Namayuni, Kibata, Mingumbi, Kinjumbi, na Somanga. Jimbo la Kilwa Kusini litakuwa na Kata ya Pande, Lihimalyao, Mandawa, Kiranjeranje, Nanjirinji, Likawage, Njinjo na Miguruwe. Pia Jimbo la Kilwa Mashariki litakuwa na Kata ya Songosongo, Masoko, kivinje, Tingi, Miteja, Kikole na Mitole.
Baadhi ya Sifa za majimbo hayo ni kama ifuatavyo. Jimbo la Kilwa Kaskazini litakuwa na wastani wa Idadi ya Watu 94, 845 na Ukubwa wa eneo ni Kilometa za Mraba 2,074.63. Jimbo la Kilwa Kusini litakuwa na wastani wa Idadi ya Watu 112,682 na Ukubwa wa Eneo ni Kilometa za Mraba 8,959.68 na Jimbo la Kilwa Mashariki litakuwa na Wastani wa Idadi ya Watu 90,149 na Ukubwa wa Eneo ni Kilometa za Mraba 2,313.18. Takwimu za Idadi ya Watu ni kwa Mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) za Mwaka 2022.
Ikumbukwe kuwa mapendekezo ya ugawaji wa Majimbo umezingatia Vigezo vyote vya Ugawaji wa Majimbo kama inavyopendekezwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa