Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainabu Telacky leo tarehe 08 Mei, 2025 amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi inayojengwa katika eneo la Kilwa Masoko, wenye thamani ya Shilingi Bilioni 266. Katika ziara hiyo, Mhe. Telacky amepata fursa ya kuzungumza na wakandarasi pamoja na timu ya wasimamizi wa mradi huo, ambapo ameelezwa kuwa hadi sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 84%.
Akizungumza baada ya kukagua hatua mbalimbali za ujenzi, Mkuu wa Mkoa ameeleza kuridhishwa kwake na kasi ya utekelezaji na ubora wa kazi inayofanyika, huku akisisitiza umuhimu wa kukamilisha mradi huo kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotarajiwa.
"Bandari hii ni miongoni mwa miradi ya kimkakati itakayochochea shughuli za uvuvi, kuongeza ajira, na kuinua kipato cha wananchi wa Lindi na maeneo jirani," amesema Mkuu wa Mkoa.
Mradi huu unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2025, na unalenga kuboresha miundombinu ya sekta ya uvuvi kwa kujenga bandari ya kisasa itakayowezesha uvuvi wa kina kirefu, usindikaji wa samaki, na usafirishaji wa mazao ya baharini kwa ufanisi zaidi.
Aidha, Serikali imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya kimkakati kama huu ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu kwa mikoa yote nchini.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa