Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mhe. Chen Mingjian, amefanya ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na China katika sekta ya uchumi wa buluu.
Ziara hiyo imefanyika tarehe 24 Juni 2025, ambapo Balozi Chen ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Mohamed Nyundo na kukagua hatua mbalimbali za ujenzi wa bandari hiyo maalum kwa ajili ya shughuli za uvuvi. Bandari hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Tanzania kuimarisha miundombinu ya sekta ya uvuvi, kuinua kipato cha wavuvi wa ukanda wa pwani, na kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye pato la Taifa.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, Balozi Chen ameeleza kuridhishwa na maendeleo ya mradi na kuahidi kuwa Serikali ya China itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza sekta ya uvuvi na maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla.
"Mradi huu una umuhimu mkubwa kwa wananchi wa Kilwa na kwa uchumi wa Tanzania kwa ujumla, China itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha kuwa miradi ya kimkakati kama hii inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa," amesema Balozi Chen.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Mohamed Nyundo, amemshukuru Balozi Chen kwa ujio wake na mchango wa Serikali ya China katika kusaidia miradi ya maendeleo nchini, pia amesisitiza kuwa bandari hiyo itakuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi wa Kilwa kwa kutoa ajira, kuimarisha biashara ya samaki, na kuongeza mapato ya halmashauri.
"Tunashukuru ushirikiano wetu na Serikali ya China kupitia mradi huu wa bandari ya uvuvi. Utekelezaji wake utaleta mapinduzi makubwa katika maisha ya wananchi wetu, hasa wavuvi na wafanyabiashara wadogo," alisema Mhe. Nyundo.
Ziara hiyo pia imeambatana na mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano kati ya pande hizo mbili, ambapo ni masuala ya uwekezaji katika sekta ndogo ndogo, na elimu ya bahari kwa jamii za pwani yalipewa kipaumbele.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa