Kilwa,
Naibu waziri wa Mifugo na uvuvi (Mb) Mhe. Abdallah Ulega amewataka wavuvi ambao bado wanaendelea na uvuvi wa kutumia Zana zilizokatazwa kuacha mara moja na kuzisalimisha kwa ajili ya kuteketezwa.
Agizo hilo amelitoa Septemba 19 alipokua akizungumza na Wavuvi na Wafugaji kata ya Somanga Wilayani Kilwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika shule ya msingi Somanga.
Ulega amesema ni vyema wavuvi wanaovua kwa kutumia zana zilizopigwa marufuku wakasalimisha Zana hizo kwa hiyari ili ziteketezwe na kuahidi kuchukuliwa hatua kali kwa wale wote watakao kaidi na kukamatwa wakiendelea kutumia zana hizo.
“Hata hapa tulipo wapo ambao wanaendelea kutumia zana ambazo zimepigwa marufuku, kama mnavyo fahamu kuwa mkono wa serikali ni mrefu ni bora ukazisalimisha kwani siku ya kukukuta hatutakuwa na msamaha dhidi yako, Mkuu wa Wilaya nikija tena naomba nikute lundo la vifaa vilivyo kamatwa ili niviteketeze na watuhumiwa ambao watakamatwa wafikishwe katika vyombo vya sheria’ alisisitiza ulega.
Pia ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kwa kushirikiana na Mradi wa usimamizi wa uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) Kujenga soko la kisasa la kuuzia Samaki katika Kata ya Somanga.
Ulega amesema iwapo Wavuvi watajengewa mazingira mazuri ya Kufanya shughuli zao watasaidia kwa kiasi kikubwa kuchangia Pato la Halmashauri.
“Mkuu wa wilaya, mkurugenzi, afisa uvuvi na wataalamu wengine na wasimamizi wa mradi wa SWIOFish naomba mshirikiane kujenga soko ambalo wavuvi hawa watauza Samaki wao na hata kujificha pindi mvua inanyesha, kaeni nao Wavuvi mjadiliane nao ni sehemu gani wanaona itakua sahihi kwa kujengwa soko
Kilwa ni miongoni mwa wilaya ambazo ziongoza kwa utaoji wa Samaki kwahiyo tukijenga mazingira mazuri itatusaidia sana katika kuongeza pato la Halmashauri” alisema Ulega.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi (Mb) Mhe. Abdallah Ulega akizungumza na Wavuvi wa Kata ya Somanga (Hawapo pichani) katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viunga vya shule ya Msingi Somanga September 19, Kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Christopher Ngubiagai na Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Ndg. Renatus Mchau (Picha : Ally Ruambo)
Aidha mhe. Ulega amewapongeza wavuvi kwa kuacha uvuvi hatarishi kwa viumbe vya baharini wa kutumia Baruti na kuwataka kuendelea na utaratibu huo.
“Uvuvi wa kutumia Baruti ulikithiri sana katika bahari ya Hindi lakini kwa sasa kwa asIlimia kubwa umepungua, tuendelee hivyo hivyo na sisi kama tutaendelea kutoa ushirikiano kuhakikisha ile hali hainjirudiii tena” alisema ulega.
Muwakilishi wa BMU Somanga akisoma risala kwa Niabu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega katika Mkutano wa hadhara wa Wafugaji na Wavuvvi uliofanyika katika Viunga vya shule ya Msingi Somanga September 19, ( Picha na : Ally Ruambo).
Katika hatua nyingine, Naibu Ulega amewataka wavuvi ambao wameanzisha makazi katika kisiwa cha Nyunni kuhama mara moja kwani kisiwa hicho sio rasmi kwa ajili ya makazi ya kudumu.
“Kisiwa Nyuni sio sehemu ya makazi kama ambavyo wavuvi wengine wanavyo fanya pale ni kwa ajili ya Dago (Mlalo) ambapo mtu anaweza kukaa siku mbili au tatu anarudi kwake, haiwezekani wengine wanakaa kabisa huko na kunywa Pombe na kuoa kabisa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Christopher Ngubiagai amemshukuru Naibu Waziri kwa ziara yake na kuahidi kuyafanyia kazi yote aliyoagiza.
Akiwa wilayani kilwa kwa ziara ya siku moja Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ailkutana na kufanya mazungumzo na wataalamu mbalimbali kutoka Halmashauri ya Wailaya ya Kilwa pamoja na kufanya mkutano wa Hadhara.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa