Shirika lisilokuwa la kiserikali la AQUA-FARMS ORGANIZATION (AFO) limefanya kikao pamoja na Viongozi wa Wilaya na Wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa ili kutoa Mafunzo na Kutambulisha Mradi wa MATUMBAWE HAI utakaohusisha Urejeshaji wa Ikolojia ya Bahari, Utalii endelevu na Ustawi wa jamii katika eneo la Ushirikiano wa Usimamizi wa Uvuvi (SOMAKI) katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa. Kikao hicho Kimefanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Kilwa, Tarehe 15/04/2025.
Akizungumza wakati wa kikao hicho Meneja wa programu wa Mradi huo, Bi. Imelda Ilomo amesema kuwa, Malengo ya kuanzishwa kwa mradi huo ni kuimarisha Miundombinu ya usimamizi wa pamoja wa Shughuli za Uvuvi katika maeneo ya SOMAKI, kerejesha Matumbawe, Kuendeleza fursa za utalii kupitia shughuli za urejeshaji matumbawe na kuongeza uzalishaji wa Pweza. Aidha ameeleza kuwa mradi huo utatekelezwa pia katika maeneo ya Songomnara, Pande, Kilwa kisiwani, Malalani pamoja na Mtitimila.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilwa Ndg. Yusuf Mwinyi amewashukuru Viongozi wa Shirika la AFO kwa maamuzi ya kuleta mradi huo Kilwa na kuahidi kuwapa ushirikiano wa hali ya juu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali waliyokusudia kuitekeleza. “Kwa niaba ya Uongozi wa Wilaya na Halmashauri kwa ujumla tumewapokea kwa moyo mkunjufu na tuko tayari kufanya kazi pamoja nanyi. Tunaomba Elimu hii mliyotoa kwetu iwafikie na wanachi ili malengo ya mradi ya kuwezesha jamii za Pwani kupitia Uchumi wa Bluu yaweze kufikiwa”.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa