“Awali nilikua naishi kwa kutanga tanga na familia yangu kwa kua sikua na uwezo wa kujenga hata kibanda cha kujistiri na familia yangu, nilikua ninaomba kuishi katika nyumba ambazo hazijamaliziwa kujengwa wenyewe wakizihitaji ninahama.
Maisha yalikuwa mabovu kwa upande wangu kwani kuna muda mpaka kula yangu na familia kwa ujumla iliku ya mashaka kutokana na kukosa pesa za kugharamia chakula”.
Maneno ya Maulidi Rashidi Hassani, mume na baba wa watoto watano aliyezaliwa miaka 34 iliyopita kijiji cha Matandu, kata ya Kivinje/Singino wilayani kilwa.
Maulidi anasema aliishi maisha duni, maisha ambayo yalikua hayamridhishi na alikua na hofu kubwa juu ya mustakabali wa maisha yake na familia yake kwa ujumla
“Kila siku nilikua ninawaza ni jinsi gani nitaondokana na hali ile niliyokua nayo, nilikua ninaihofia sana kesho yangu. Kazi nilikua nafanya lakini kipato kilikua hakikidhi mahitaji kwahiyo nilikua nashindwa hata kujiwekea kiasi Fulani kwa ajili ya kuanzishi miradi ya maendeleo” anasema Maulidi
Bw. Mauilidi Rashidi akizungumza na mratibu wa Tasaf Wilaya ya Kilwa Kilwa Bi. Stella Omari Kashingo alipomtembelea kupata tathimini jinsi ya Mpango wa kunusuru kaya masikini jinsi ulivyo Masaidi (Picha na Ally Ruambo).
Maulidi anasema kwa sasa maisha yake yamebadilika baada ya Mfuko wa maendeleo ya jamii (Tasaf) kumuwezesha kujikwamua kutoka katika umasikini ulio kithiri mpaka sasa anaweza kusimama imara kama baba wa familia.
“Aisee kwa sasa mimi sio Maulidi yule wa zamani maisha yangu yamebadilika kwa asilimia kubwa. Siwezi kusema kuwa sina shida hapana shida tumeumbiwa binadamu lakini nashukuru sasa niko vizuri kwani nimeweza kununua kiwanja kwa pesa yangu na kujenga kibanda changu ingawa sio cha kudumu ila siku zote safari moja uanzisha nyingine(anacheka)”.
Ni njinsi gani Mfuko wa maendeleo ya jamii umesaidia kubadili maisha ya maulidi na familia yake?
Maulidi anasema alitambuliwa na kuingizwa katika mpango wa kunusuru kaya masikini ambapo alianza kupokea kiasi cha shilingi Elfu Thelathini na sita kila baada ya miezi miwili pesa ambayo aliigawa mara mbili.
Anasema shilingi elfu kumi na sita aliitumia kwa ajili ya chakula na kiasi kinachobaki aliitumia kukodi mashine ya umwagiliaji kwa ajili ya bustani ya mboga mboga aliyo ianzisha baada ya kuanza kupata ruzuku.
“Mpaka leo ruzuku yangu siitumii yote kwa ajili ya chakula, nikiipata tu uwa naigawa mara mbili elfu kumi na sita naitumia kwa chakula au masuala ya shule ya watoto wangu kama vile kununua Madaftari, peni na vitu vingine vidogo vidogo inayobaki naitumia katika mradi wangu wa bustani”.
Maulidi anasema baada ya kuanza kuuza mboga mboga mtaji wake ulikua na kuamua kuanzisha mradi mwingine ambapo alimpatia mke wake kiasi cha pesa ambacho alikitumia kwa kuanzisha biashara ya vitumbua.
“Mke wangu ninashirikiana nae katika shughuli za kuhudumia bustani lakini pia nimempatia pesa kidogo ambazo anafanyia biashara ya vitumbua. Namshukuru Mungu biashara inaendelea vizuri kwani tunapata pesa ambayo inasaidia kukidhi mahitaji madogo madogo kwani hata kama mda wakupata ruzuku unakua haujafika uwa hatuyumbi katika swala la chakula”
Anasema pia tasaf walimpatia mradi wa mbuzi watano ambao amewafuga kwa muda mpaka sasa anaendelea nao na wamekua msaada mkubwa sana katika maisha yake.
“Pia nina mradi wa kufuga mbuzi ambao lipatiwa na Tasaf, walinipatia mbuzi watano na mpaka sasa nina mbuzi zaidi ya Ishirini na saba. Wengine uwa nauza kwa ajili ya kuweza kuwahudumia kwani wakiwa wengi sana inakuwa shida katika kuwahudumia hasa katika swala la madawa.
Baadhi ya Mbuzi wa Bw. Maulidi ambao ni miongoni mwa matunda ya Mfuko wa maendeleo ya jamii (Tasaf) Picha na Ally Ruambo.
Hapa nimebakisha wachache kutokana na ufinyu wa eneo langu wengine nimewajengea kule chini ambako uwa naenda kuwaangalia kila siku.
Pesa ninazozipata baada ya kuuza hawa mbuzi huwa natatulia matatizo yangu pamoja na kuhudumia watoto wangu katika elimu lakini pia nina nunua madawa kwa ajili ya kutibu hawa mbuzi wapatapo magonjwa”
Lakini pia ninashiriki katika ajira za muda katika miradi mbalimbali inayoendeshwa na Tasaf kama sasa hivi kuna ujenzi wa Rambo hapa kijijini kwahiyo na mimi ninashiriki katika shughuli hizo ambazo zinaniongezea kipato ukiachana na shughuli zangu zingine.
Bw. Rashidi anasema kua anajivunia kuwa miongoni mwa wanufaika wa mpango wa kuokoa kaya masikini kwani umeacha alama kubwa sana katika maisha yake na familia yake kwa ujumla.
“najivunia kuwa mnufaika wa mpango kwani nimeweza kujiinua kiuchumi lakini pia nimeweza kununua eneo na kujenga nyumba ya kuishi ingawa sio ya kudumu lakini inanifaa tofauti na zamani nilipokua nikitangatanga” alisema Rashidi
Rashidi anaishauri serikali iendelee na Mpango wa kunusuru kaya masikini na mipango mingine zaidi kwa watu wenye mahitaji na kuwashauri walio kwenye mpango kuzitumia ruzuku kwa kufanyia mambo ya msingi.
“Serikali iendelee na Mpango wa kunusuru kaya masikini na mipango mingine zaidi kwa watu wenye uhitaji kama sisi mana sio sisi tu tuna huo uhitaji kunawengine pia wanahitaji ili waweze kujikwamua kimaisha lakini na walengwa wa mpango wasijisahau wazitumie hizo pesa vizuri ili ziwaletee matokeo chanya” alisisitiza Rashidi
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa