Kilwa,
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mh. Christopher Ngubiagai amezindua rasmi zoezi la utoaji wa Chanjo dhidi ya saratani ya Mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14.
Uzinduzi huo umefanyika mapema leo katika viunga vya Shule ya Msingi Ukombozi Mjini Kilwa Masoko ambapo zaidi ya wasichana 120 kutoka Shule nne walipatiwa huduma hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Christopher Ngubiagai akitaarisha Chanjo kuashiria kuzinduliwa rasmi kwa zoezi la utoaji wa Chanjo dhidi ya Saratani ya Mlango wa kizazi wilayani Kilwa ( Picha na Ally Ruambo)
Awali akihitimisha kikao cha Afya ya Msingi Wilaya, kilichokaa kujadili mambo mbalimbali ikiwemo zoezi zima la utoaji Chanjo na Somo kuhusu saratani ya Mlango wa Kizazi, Mh. Ngubiagai amewataka Wajumbe kuwa Mabalozi wazuri katika jamii kwa kutoa elimu sahihi juu ya umuhimu wa Chanjo dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi.
Aidha, amewataka wale wenye umri juu ya miaka 14 kwenda kwenye vituo vya afya kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa awali.
“Pia tukawaelimishe wale ambao umri wao ni zaidi ya miaka 14 waende katika Vituo vya afya kwa ajili ya uchunguzi wa awali, na iwapo watathibitika kuwa wana matatizo basi waanze matibabu mapema” alisema Ngubiagai
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Christopher Ngubiagai akimkabidhi kadi mmoja wa wanafunzi waliojitokeza katika viunga vya Shule ya Msingi Ukombozi baada ya kupatiwa chanjo dhidi ya Saratani ya Mlango wa kizazi (Picha na Ally Ruambo).
Jumla ya Wasichana 3378 kutoka kata mbalimbali Wilayani Kilwa wanatarajiwa kupatiwa Chanjo dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi duru ya kwanza, ambapo 2790 kati yao ni wanafunzi kutoka shule za Msingi na Sekondari.
Chanjo ya kujikinga na saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye miaka 14 utolewa mara mbili ambapo mtoto upatiwa tena chanjo baada ya miezi 6 kutoka tarehe ya chanjo ya kwanza
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa