Wadau mbalimbali wa sekta za umma na binafsi wamepatiwa mafunzo ya matumizi ya Mfumo wa Usimamizi na Ununuzi wa Umma Kielektroniki (NeST), unaoratibiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kanda ya kusini. Mafunzo hayo yametolewa kwa siku mbili huku yakilenga kuongeza uelewa na uwezo wa washiriki katika kutumia mfumo huo kwa usahihi, ili kuhakikisha michakato ya manunuzi inafanyika kwa uwazi, uwajibikaji na kwa ufanisi zaidi.
Mafunzo hayo yamefanyika Tarehe 15 na 16 Agosti 2025 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa ambapo washiriki wamejifunza namna mfumo wa NeST unavyorahisisha uwasilishaji wa zabuni, kupanua fursa za ushiriki kwa wazabuni wengi na kuhakikisha matarajio ya watumiaji yanakidhiwa. Vilevile, mfumo huu unalenga kuhakikisha thamani halisi ya fedha katika michakato ya manunuzi ya umma.
Faida kubwa ya matumizi ya mfumo wa NeST ni pamoja na kupunguza muda wa taratibu za manunuzi kwa kuondoa urasimu usio wa lazima, kuongeza usalama wa taarifa, pamoja na kuimarisha kasi ya uwasilishaji na upokeaji wa nyaraka muhimu. Hatua hii inasaidia kuongeza tija kwa taasisi za umma na binafsi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa ujumla, NeST imebuniwa kama chombo madhubuti cha kuimarisha upatikanaji wa taarifa kwa wakati, kuongeza ushiriki wa wadau mbalimbali, na kuhakikisha uwazi katika mnyororo mzima wa ununuzi wa umma nchini. Kupitia matumizi ya mfumo huu, Serikali inalenga kujenga mfumo wa manunuzi wa kisasa unaoendana na teknolojia na mahitaji ya sasa ya kiutawala.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa