Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, chini ya Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), imekabidhi chanja 40 za kisasa kwa wavuvi wa dagaa katika eneo la Kilwa Kivinje, mkoani Lindi. Chanja hizo zenye thamani ya shilingi milioni 117 zinalenga kuboresha uhifadhi wa dagaa baada ya kuvuliwa.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi miundombinu hiyo iliyofanyika tarehe 21 Agosti 2025 wilayani Kilwa, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi na kuhakikisha dagaa zinazovuliwa zinakaushwa katika mazingira salama na yenye kuzingatia viwango vya usalama wa chakula.
“Ninatambua kuwa hapo awali dagaa mnaovua hapa walikuwa wakiharibika kutokana na kukaushwa kwenye miundombinu isiyo rafiki. Wakati mwingine walikutwa na mchanga jambo ambalo lilipunguza thamani sokoni na kuhatarisha afya ya walaji. Hatua hii itamaliza changamoto hizo zote,” alisema Mhe. Dkt. Kijaji.
Aidha, Waziri Kijaji aliwataka wavuvi kuhakikisha wanaitunza na kutumia miundombinu hiyo ipasavyo ili iweze kuwanufaisha kwa muda mrefu na kufanikisha malengo yaliyokusudiwa na Serikali.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa