Kamati ya Lishe ya Wilaya ya Kilwa imefanya kikao tarehe 21 Agosti 2025 katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii (FDC) – Kilwa, kwa lengo la kujadili utekelezaji wa shughuli za lishe kutoka idara na vitengo mbalimbali kwa kipindi cha Aprili hadi Juni 2025.
Katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Ndugu Matiko Kebaha ametoa msisitizo kwa wajumbe wa kamati kutekeleza kwa vitendo afua za lishe, badala ya kubaki kwenye maandiko ya mipango pekee. Ametoa wito wa kuanzishwa kwa mashamba darasa ya mfano yanayosimamiwa na Halmashauri, pamoja na kuhakikisha kuwa kila shule inakuwa na shamba la chakula ili kuchangia upatikanaji wa lishe bora kwa wanafunzi.
Aidha, amehimiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Halmashauri na wadau mbalimbali katika kutatua changamoto zinazohusiana na lishe mashuleni, kwa lengo la kuboresha afya na maendeleo ya watoto.
Vilevile, kikao kimeweka mkazo katika kuhakikisha kaya zote katika Halmashauri zinakuwa na vyoo safi na salama, kama hatua muhimu ya kudhibiti magonjwa ya mlipuko na yale yanayotokana na uchafu wa mazingira.
Kikao hiki ni sehemu ya utekelezaji wa mkataba wa lishe wa wilaya na dhamira ya dhati ya Halmashauri katika kuboresha hali ya lishe na afya ya jamii wilayani Kilwa.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa