Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe.Christopher Ngubiagai amewataka waheshimiwa madiwani kuhakikisha wanaisimamia Halmashauri kwa ukaribu ili kupunguza malalamiko ya wananchi. ‘’Waheshimiwa madiwani, nyie ndiyo wasimamizi wakuu wa Halmashauri, hakikisheni mnasimamia ukusanyaji wa mapato na pia kuhakikisha kile kinachokusanywa kinafanya kazi kulingana na bajeti, msipofanya hivyo haya malalamiko ya wananchi kuhusu huduma mbali mbali yataendelea kuwepo siku hadi siku’’ alisisitiza Mhe.Ngubiagai.
Mhe.Mkuu wa Wilaya pia aliwataka Wahe.madiwani katika maeneo yao kuhakikisha wanadhibiti uingizaji holela wa mifugo katika kata zao kwani ni changamoto mpya katika Wilaya yetu ambapo kumekuwa na wimbi kubwa la mifugo inayoingizwa kutoka mikoa mbali mbali. ‘’Wilaya yetu ni kubwa , hivyo bila kupata taarifa sahihi na kwa wakati kutoka kwenu hatuwezi kujua ni kijiji gani kuna changamoto ya mifugo ili wenye mamlaka tuweze kuchukua hatua kwa wakati’’ aliongeza Mhe.Mkuu wa Wilaya.
Mkuu wa Wilaya alisistiza kuwa kimsingi hawazuii mifugo kuingia katika Wilaya ya Kilwa isipokuwa ni lazima tujua ni mfugaji gani yupo wapi na idadi ya mifugo pia ilingane na maeneo yaliyotengwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Mhe.Farida Kikoleka aliwahimiza wataalam wa Idara mbali mbali ndani ya Halmashauri kuhakikisha kila mmoja anawajibika katika nafasi yake bila kujali changamoto zilizopo. ‘’Najua mna changamoto mbali mbali hasa idara za Afya na Elimu kutokana na upungufu wa watumishi, lakini bado mna wajibu wa kufanya kazi kwa bidii kwa sababu wananchi wana matumaini makubwa na nyie’’ alisisitiza Mhe.Kikoleka.
Naye Kaimu Mkurugenzi Bw.Godfrey Jaffari aliwahakikishia waheshimiwa madiwani kuwa timu yake itaendelea kufanya kazi kwa weledi na kufuata maelezo ya Waheshimiwa madiwani na kushauri pale watakapohitajika kulingana na nafasi zao. ‘’ tumeyasikia maelekezo ya Mhe.Mkuu wa Wilaya , tumeyasikia maelezo ya waheshimiwa madiwani pia , nawaahidi tutayafanyika kazi’’ aliongeza Bw.Jaffari.
Katika baraza hilo kamati za kudumu ziliwasilisha taarifa zao katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi 2021 ambapo kamati ya fedha, Uongozi na Mipango iliwasilisha taarifa ya mapato na matumizi ambapo kiasi cha shilingi Bilioni 1.3 ilikusanywa kutoka vyanzo mbali mbali vya ndani, wafadhili na serikali kuu na mpaka Mchi 31 Jumla ya shilingi milioni 903 ilitumika katika matumizi ya kawaida na miradi mbali mbali kama ujenzi wa madarasa, vyoo, ununuzi wa madawati pamoja na utoaji wa ruzuku kwa kaya masikini chini ya mpango wa kunusuru kaya masikini-TASAF. Kamati zingine zilizowasilisha taarifa zao ni Kmati ya Uchumi , ujenzi na mazingira, Kamati ya Elimu, Afya na Maji pamoja na Kamati ya Kudhibiti Maambukizi ya Ukimwi.
Wilaya ya Kilwa inaundwa na Tarafa sita ,kata 23 pamoja na vijiji 91 ambapo vyanzo vikuu vinavyochangia mapato ya ndani ni uvuvi, kilimo cha Ufuta na Korosho pamoja na uchimbaji wa madini ya gypsum.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa