Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Ofisi ya Raisi (TAMISEMI) na Jeshi la Polisi Tanzania,imetoa mafunzo ya Uraia na Utawala bora kwa viongozi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa lengo ikiwa ni kuwakumbusha viongozi hao kuzingatia haki za binadamu, usalama na misingi ya utawala bora katika utendaji wa majukumu yao.
Mafunzo hayo yametolewa leo tarehe 04/03/2025 Katika Ukumbi wa Sultani Kilwa Masoko ambapo mwezeshaji ACP Elisante Ulomi ametoa elimu juu ya ulinzi na usalama wa Nchi na kuwahimiza viongozi ngazi ya Mitaa kuielimisha jamii juu ya kushiriki katika kulinda amani na usalama kwa kujiunga na makundi mbalimbali ya ulinzi na usalama, pia kuwa wazalendo kwa kutoa taarifa za uhalifu unaojitokeza katika mazingira yao, ili kuhakikisha vitendo hivyo vinaondolewa na usalama unaimarika katika jamii.
Pia akiwasilisha mada ya Madaraka kwa Umma Ndg. Hamisi Ujanja amewahimiza viongozi wa Serikali za Mitaa na watumishi wa Halmashauri kushirikisha wananchi katika utekelezaji wa miradi ya serikali ili kupunguza malalamiko na kujenga dhana ya uwajibikaji na utawala bora.
Kwa upande wake Ndg.Yohana Mcharo amesema moja ya malengo ya mafunzo hayo ni kuwakumbusha watendaji ngazi ya Serikali za Mitaa juu ya umuhimu wa kuelewa muundo wa serikali za Mitaa na kutimiza wajibu wao kupitia sheria zinazoongozwa na serikali hiyo ili ya kutimiza lengo la utawala bora.
Akizungumza katika mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Mohamed Nyundo ametoa shukrani kwa Wizara ya katiba na Sheria kwa kutoa elimu ambayo inasaidia viongozi kuwa bora na kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kuzingatia misingi ya sheria na utawala bora, Pia amewataka Maafisa Watendaji kata na Wakuu wa Idara wa Hamashauri waliohudhuria katika mafunzo hayo kufikisha elimu walioipata katika jamii ili kuweza kufikia malengo ya elimu hiyo.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa