Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa amewataka wananchi wote nchini kuhama kutoka maeneo ambayo yameonekana ni hatarishi kwa makazi hasa katika kipindi hiki cha Mvua.
Mhe.Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo katika ziara yake ya kikazi ya siku moja wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi. Ziara hiyo ya Waziri Mkuu ililenga kuwapa pole wahanga wote wa mafuriko katika mkoa wa Lindi kwa ujumla ambapo athari kubwa za mafuriko hayo yametokea katika Wilaya ya Kilwa yenye athari katika vijiji kumi na saba (17) ndani ya kata saba za Wilaya ya Kilwa.
Akiwa Wilayani Kilwa Mhe.Waziri Mkuu alipata fursa ya kukagua athari za mafuriko kwa njia ya anga na kisha kufanya mikutano miwili ya adhara katika Vijiji vya Nakiu katika kata ya Nanjirinji na Kijiji cha Kipindimbi iliopo kata ya Njinjo.
Katika kata ya Njinjo, Mhe.Waziri Mkuu alitembelea eneo lililoathirika na kisha kukutana na wananchi ambapo alifikisha salamu pole za Serikali kutoka kwa Mhe.Dr.John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania ambapo aliwahakikishia wananchi hao kuwa Mhe.Rais ameguswa na maafa ya watu 13 yaliyotokea katika Wilaya ya Kilwa pekee na Zaidi ya kaya 3774 zilizokosa makazi kutokana na mafuriko hayo yaliyoanza tarehe 26Januari 2020.
‘’Nimeona hali halisi ya mafuriko, ni janga kubwa ,nawasihi viongozi wa Wilaya na Mkoa mshirikiane kwa pamoja kuhakikisha wananchi hawa wanapatitiwa viwanja katika maeneo salama lakini pia hawarudi katika maeneo ya mabondeni’’ alisisitiza Mhe.Waziri Mkuu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe.Christopher Ngubiagai alimhakikishia Mhee.Waziri Mkuu kuwa Ofisi yake itasimamia upatikanaji wa viwanja maeneo salama ambapo mpaka kufikia tarehe 5Januari 2020 jumla viwanja 670 vilishapimwa na kugawanywa kwa wananchi na tayari baadhi ya wananchi wameshaanza ujenzi katika maeneo hayo.
Mkuu wa Wilaya pia alitumia nafasi hiyo kumweleza Mhe.Waziri mkuu ukubwa wa maafa hayo ambapo Zaidi ya wananchi elfu tisa bado ni wahitaji wa huduma muhimu za kijamii kama chakula na malazi kwa sababu wengi wao walipoteza mali zao zote na kwa sasa pamoja na kupatiwa viwanja lakini mpaka sasa bado wanapatiwa msaada wa chakula na malazi kutoka Ofisi ya Wilaya kutokana na uharibifu uliotokea.
Mhe.Waziri Mkuu alimhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa ofisi yake imeshafanya tathmini na tayari imeshachukua hatua ya kuleta misaada ya kijamii.
Katika Wilaya ya Kilwa Mfuriko yalitokea kuanzia tarehe 26 Januari 2020 ambapo Jumla ya kaya 3774 yenye jumla ya wanannchi Zaidi ya 24,000 ziliathirika ambapo wananchi walipoteza mali zao, nyumba zao, mifugo pamoja na mazao.
Kata zilizoathirika Zaidi ni kata za Njinjo, Mitole, Kikole, Mandawa na Kiranjeranje. Kata zingine ni Nanjirinji na Kivinje. Kati ya wananchi 24,000 waliothiriwa, wananchi 9860 wamekuwa wakiishi katika kambi na vituo mbalimbali kwa kutegemea misaada yote ya kibinadamu na kijamii katika vituo hivyo na katika maeneo salama walipohamishiwa.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa Wilaya ya Kilwa ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Ndg Renatus Mchau alimweleza Mhe.Waziri Mkuu kuwa Ofisi yake inaendelea kuratibu misaada yote inayotolewa na Serikali na wadau mbali mbali na kuhakikisha kuwa misaada hiyo inawafikia walengwa ambao ni waathirika wa mafuriko kwa wakati.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa