Kilwa,
Ikiwa imepita wiki moja toka vikundi vya usimamizi shirikishi wa rasilimali za bahari wilaya ya Kilwa kuelekeza vilio vyao kwa Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi juu ya ukosefu wa Boti za kufanyia doria Hatimaye vilio vyao vyapatiwa ufumbuzi.
Ufumbuzi huo umepatikana Septemba 26, baada ya Umoja wa Ulaya (EU) kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi mazingira (WWF) Tanzania kukabidhi msaada wa boti mbili zenye uzito wa tani 1.6 kila moja ambazo zimegharimu Dola za kimarekani 64,015 sawa na Shilingi 144,033,750 ikiwa pamoja na gharama ya injini zenye horsepower 40 kila moja na vifaa vya usalama majini kwa Vikundi vya Bmu vya wilaya ya kilwa (CFMA ya TIM4SI) na Wilaya ya mafia makabidhiano yaliyofanyika katika viwanja vya Maalim Seif Mjini Kilwa Kivinje.
Akizungumza katika makabidhiano ya Boti hizo Mkurugenzi wa Shirika la kuhifadhi Mazingira (WWF) Tanzania Dokta Amani Ngusaru amesema Boti zilizoltolewa ni kwa ajili ya ulinzi wa mazingira na rasilimali za uvuvi na kuvitaka vikundi hivyo kuzitumia kwa Malengo yaliyo kusudiwa.
“Hizi boti zikatumike kwa uangalifu na kwa malengo ambayo yamekusudiwa hizi boti ni kwa ajili ya kufanyia doria na si kwa ajili ya uvuvi’’ alihitimisha Dokta Ngusaru
Moja ya Boti zilizokabidhiwa kwa Vikundi vya usimamizi shirikishi wa rasilimali za Bahari wilaya ya Kilwa kwa ajili ya Doria
Naye Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amewapongeza wananchi wa Kilwa Kivinje kwa kukubali kubadilika na kuachana na uvuvi haramu wa kutumia Mabomu na kuagiza vikundi vya usimamizi shirikishi wa rasilimali za bahari kuwakamata wote ambao wanajihusisha na uvuvi wa kutumia zana zilizo katazwa na kuwafikisha katika vyombo vya sheria bila kuwaonea huruma.
“Hao waliokuwa wanapiga mabomu ndio wamesababisha mapaka leo kuanzia tanga hadi Mtwara hakuna kiwanda cha samaki, nani anaweza kuwekeza sehemu ambayo hana uhakika wa malighafi atazipata wapi, Ninyi mpo kisheria fanyeni kazi zenu bila kuogopa vitisho kutoka kwa mtu yeyote. Kamateni wote ambao wanafanya uvuvi haramu na muwafikishe katika vyombo vya sheria mkishindwa kuwadhibiti nipeni taarifa” alisema Ulega
Aidha ameitaka Halmashauri kuvipa vikundi mamlaka ya kukusanya Ushuru ili vikundi hivyo viweze kujiendesha vyenyewe bila kuitegemea Halmashauri katika kujiendesha.
“Kabla ya kuja hapa nilikuwa Pangani Tanga na wameniambia kuwa Bmu zimepwa majukumu ya kukusanya ushuru na asilimia wanazozipata kama malipo zinatumika kujiendesha, kabla ya kupewa jukumu hilo makusanyo yalikuwa kati ya Milioni Thelathini lakini toka wapewe majukumu ya kukusanya yamepanda hadi Milioni Mia mbili sasa na hapa nataka muige huo mfano nikija tena mwezi wa kumi na moja nikute hilo limefanyika” alihitimisha Ulega.
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa Halmashauri yaa wilaya ya kilwa Ndg. Pundile ameishukuru Shirika la kuhifadhi Mazingira (WWF) kwa msaada wa boti ambazo zitasaidia katika kuimarisha ulinzi katika bahari ambayo Halmashauri inaitegemea kama moja ya chanzo chake cha mapato.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa