Kilwa,
Wanawake nchini wametakiwa kuto fumbia macho vitendo vya kikatili vinavyofanywa dhidi yao badala yake watoe taarifa katika vyombo vya sheria na asasi zingine zinazo jishughulisha na kutetea haki za wanawake.
Wito huo umetolewa na Katibu tawala wilaya ya kilwa Bw. Haji Mbaruku Balozi alipokua akihutubia wananchi kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya kilwa katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika wilayani kilwa katika viwanja vya Garden Mkapa.
Bw. Balozi amesema iwapo vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake vitaendelea kufumbiwa macho katika jamii basi madhara makubwa yataendelea kutokea ikiwemo kukosa haki zao za kimsingi ambazo zinapelekea kurudisha nyuma gurudumu la maendeleo.
Amesema serikali wilayani kilwa iko macho na imejipanga kuhakikisha inawachukulia hatua kali za kisheria wale wota ambao watabainika na kukutwa na hatia ya kutenda vitendo vya kikatili na unyanyasaji wa aina yeyote ile dhidi ya wanawake na watoto.
“Katibu wa jukwaa la wanawake naomba tushirikiane katika hili, lete matatizo ya wanawake ambayo mmekua mkikutana nayo huko mnakopita ili kwa pamoja tuone ni jinsi gani tunawasaidia ”. Alisisitiza Bw. Balozi
Pia amewataka wanawake kuanzisha na kuvisajiri vikundi katika mamlaka husika ikiwemo Mamlaka ya Mapato (TRA) ili viweze kutambulika kisheria na kuahidi kuwaomba Mamlaka ya Uthibiti Ubora (TBS) kuja wilayani kilwa kwa dhumuni la kuvijengea uwezo vikundi ambavyo vimekua vikijishughulisha na usindikaji wa vyakula ili kuongeza thamani ya bidhaa zao.
Katibu Tawala Wilaya ya Kilwa Bw. Haji Mbaruku Balozi akihutubia wananchi katika kilele cha siku ya Wanawake Dunia iliyofanyika katika viwanja vya Garden Mkapa mjini Kilwa Masoko.
Aidha amewataka wanawake kujitokeze kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika chaguzi zinazotarajiwa kufanyika mwaka kesho na uchaguzi mkuu, kwani wanauwezo mkubwa wa kuongoza kama ambavyo wanawake wengine wamekua wakiongoza wizara mbalimbali.
Akisoma Risala ya maadhimisho ya siku ya wanawake Kwa niaba ya wanawake wa wilaya ya kilwa Bi. Nuru ameimba serikali kupitia mgeni rasmi kuwatafutia masoko ya uhakika kwa ajili ya kuuza bidhaa zao ambazo wanazitengeneza pamoja na kuimarishiwa miundo mbinu kwani miundo mbinu iliyopo sasa hairidhishi.
Nae muwakilishi kutoka Dawati la jinsia wilaya ya kilwa Wp. Mackrina ameiomba jamii ishirikiane na Dawati hilo kwa kuripoti vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake na watoto na kuacha tabia ya kuficha vitendo hivyo au kumalizana kienyeji.
Awali akitoa salamu zake Katibu wa Jukwaa la wanawake Kilwa Bi. Pili Mohamedi amewataka wanawake waungane katika kupinga ukatili dhidi yao na kuzikabili changamoto mbalimbali katika kuleta ukombozi.
Pia ameishukuru idara ya maendeleo ya jamii wilayani kilwa kwa kuwajengea uwezo katika kufanikisha shughuli zao za kila siku katika kuhakikisha mwanamke anapata haki zake anazostahili.
Kila tarehe 8 machi Tanzania inaungana na nchi nyingine wanachama wa umoja wa mataifa kuadhimisha siku ya wanawake duniani. Kauli mbiu ya kitaifa kwa mwaka 2018 ni “Kuelekea Uchumi wa Viwanda, Tuimarishe Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji Wanawake Vijijini.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa