Taasisi ya Umoja Pamoja imeendelea kuunga mkono jitihada za kukuza ustawi wa michezo wilayani Kilwa kwa kuandaa eneo la michezo mbalimbali. Eneo hili linajumuisha viwanja vya mipira kama mpira wa kujipanga (pick-up ball), mpira wa wavu (volleyball), na netiboli (netball), lengo ikiwa ni kuendeleza na kukuza shughuli za michezo kwa jamii na vijana Kilwa.
Maafisa kutoka Kitengo cha Tamaduni, Sanaa na Michezo wametembelea eneo hilo lililopo Ngome Masoko Tarehe 07 Oktoba 2025 kujionea maendeleo ya ujenzi ili kuhakikisha vijana watapata nafasi ya kushiriki kikamilifu katika michezo na shughuli za kijamii.
Mbali na maendeleo ya michezo, Taasisi ya Umoja Pamoja imepanga pia kujenga madarasa ya ujasiriamali, ikiwemo kilimo na ufugaji, ili kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa vitendo na kuongeza kipato. Hatua hii inalenga kukuza uchumi wa vijana na jamii kwa ujumla.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Umoja Pamoja Bwana Metthew Nkusa amesema
"Dhamira yetu kuu ni kuandaa eneo rafiki kwa vijana litakalowawezesha kukutana kwa ajili ya michezo, kujenga umoja, na kubadilishana mawazo chanya yatakayowasaidia kufikia maendeleo."
Kwa upande wao, maafisa Utamaduni, Sanaa na Michezo wameipongeza Taasisi ya Umoja Pamoja kwa jitihada zao katika kukuza michezo na shughuli za kijamii kwa vijana wilayani humo.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa