BILIONI 100 KUMALIZA TATIZO LA MAJI KILWA
Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Maji Prof.Makame Mbarawa katika ziara siku moja aliyoifanya Wilaya ya Kilwa taehe 27Septemba 2019,Ziara hiyo ya Mhe.Waziri ililenga kufikisha ujumbe wa serikali kwa wananchi wa Wilaya ya Kilwa kwa ujumla juu ya tatizo la upatikanaji wa maji ya uhakika.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe.Christopher Ngubiagai akisoma taarifa ya Wilaya juu ya upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Kilwa yenye ukubwa wa Kilometa za 13,290 na wakazi wanaofikia 203,000. Mhe.Mkuu wa Wilaya alimueleza Mhe.Waziri kuwa hali ya upatikanaji wa maji kwa sasa si ya kuridhisha kwani ni asilimia 62 tu ndiyo inayopata maji kwa maeneo ya mijini na asilimia 59 kwa vijijini.
Mhe.Mkuu wa Wilaya alileza pia mipango iliopo kuwa mradi mkubwa kutoka mto Mavuji unaotarajia kutumia jumla ya shilingi 1.38 trilioni, huku mpango wa muda mfupi ukiuwa ni kuchimba visima saba katika vijiji na vitongoji saba. Mkuu wa Wilaya pia alieleza kuwa kwa sasa kuna jumla ya visima 408 vinavyotumia pampu za mikono huku visima vinavyofanyakazi vikiwa 335 tu.
Mkuu wa Wilaya pia alieleza Changamoto zinazoikabili Wakala wa Usambazaji na usafi wa Mazingira katika Wilaya ya Kilwa (RUWASA) kuwa ni pamoja na baadhi ya taasisi za serikali kutolipa bili kwa wakati pamoja na uharibifu wa miundombinu za maji hasa katika maeneo ya vijijini.
Baada ya kupokea taarifa hiyo Mhe.Mbarawa alieleza mipango ya serikali ya muda mrefu na mfupi kuwa ni kuchimba kisima kirefu katika hospitali ya Kinyonga katika mji mdogo wa Kivinje na mpango wa muda mrefu wa kutoa maji kutoka mto Mavuji unaofadhiliwa na serikali ya India unaotarajiwa kuanza Disemba mwaka huu 2019.
Akiwa katika kikao cha hadhara katika mji mdogo wa Kilwa-Kivinje Mhe.Mbarawa aliwaahidi wananchi hao kuwa tatizo la maji sasa litakuwa limefika mwisho. “Ndugu wananchi sitowi ahadi hii mbele yenu tu bali natoa ahadi hii mbele ya Mwenyezi Mungu aliyenipa nafasi ya kufika hapa leo kuongea nanyi” alisema Prof.Mbarawa.
Kwa upande wake Mbunge wa Kilwa Kusini Mhe.Selemani Bungala maarufu kama Bwege alimshukuru Mhe.Mbarawa na kuwaambia wananchi kuamini yote aliyowaahidi kwani ni mtu mkweli na muugwana, “Ndugu zangu wana Kilwa, Huyu Bwana ni mtu mkweli na muungwana kweli kweli, tumuombee Mwenyezi Mungu ampe afya njema ili yote aliyotuahidi yakamilike kwa wakati” aliongeza Mhe.Bungara.
Awali Mhe.Prof.Mbarawa akiongea na watumishi wa Wilaya ya Kilwa katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya aliwasisitiza kufanya kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu wa hali ya juu ili kuwaletea wananchi kile wanachotarajia kukipata. “Niwaombe watumishi wenzangu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.John Pombe Magufuli nataka kuona matokeo ya kile kinachofanyika na si hizi taarifa nzuri mnazotuandikia, anataka kuona mnawaondolea wananchi kero zao, hii si karne ya kutembea nan doo kichwani kilomita tano kufuata maji” alisisitiza Mhe.Mbarawa. Aliongeza kuwa “Katika taarifa yenu nimeona upungufu wa watumishi katika Idara wa Maji, lakini naomba waliopo wafanye kazi kwa kwa bidi wakati tukiendelea kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo”.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa