Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Mohamed Nyundo amewataka Maafisa Watendaji Ngazi za Kata kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia swala la lishe katika kata na vijiji wanavyofanyia kazi. Hayo ameyasema wakati wa kikao cha Tathmini ya Mkataba wa Lishe Ngazi ya kata na Vijiji kilichofanyika katika ukumbi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya kilwa tarehe 23/10/2024.
Katika utekelezaji wa hatua hiyo Mhe. Nyundo amewaagiza Watendaji hao kutoa elimu ya lishe kwa Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji ili kuhakikisha wanaelewa umuhimu wa lishe kwa watoto mashuleni na jamii wanayoongoza. Pia amewaagiza watendaji hao kuhakikisha wanajipanga vizuri kutoa elimu ya lishe kwa wananchi kupitia mikutano au matukio mbalimbali ya kijamii ili kuwahamasisha wazazi kuchangia kiasi cha fedha ili kuwawezesha wanafunzi kupata chakula wawapo mashuleni. “ukienda kanisani sema, ukienda msikitini sema, ukienda kwenye tukio la michezo sema”
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya Ndg. Ernest Shirima amesema Halmashauri kupitia Idara ya Afya, Elimu na Idara Nyingine Mtambuka inajipanga kuja na mkakati mzuri utakaotumika kuhakikisha inaboresha na kusimamia suala la lishe mashuleni.
Aidha Mhe. Nyundo ameipongeza Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa kwa kutoa kiwango stahiki cha fedha kwa ajili ya utekelezaji wa afua za lishe.Pia ametoa wito kwa ofisi hiyo kuendelea kutoa fedha kwa kuzingatia umuhimu wa lishe kwa watoto mashuleni na jamii kwa ujumla.
Katika kuitimisha kikao hicho Mhe. Nyundo ameweka msisitizo kwa kuendelea kufanya juhudi za kumaliza changamoto ya mlipuko wa kipindupindu, ambapo amemuelekeza Mkurugenzi Mtendaji kupita Ofisi ya Mganga Mkuu kutoa elimu kwa watendaji juu ya choo bora na kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi wote.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa