Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Ndg Renatus Mchau leo ameungana na wananchi, wakuu wa idara, wataalam na viongozi wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Masoko katika ujenzi wa shule mpya sekondari katika Kata ya Masoko.
Ujenzi huo ni sehemu ya ujenzi wa madarasa 20 katika shule za 11 zenye upungufu wa madarasa kwa wanafunzi ambao wameanza kupokelewa kuanzia tarehe 06, Januari mwaka huu. Upungufu huu wa madarasa umetokana la ufaulu wa wanafunzi kuongezeka ukilinganisha na maoteo ya awali ambapo jumla ya vyumba vinavyohitajika ni 65 ikiwa Halmashauri kwa kushirikiana na wananchi walikua wamekamilisha ujenzi wa vyumba 45 vilivyotokana na maoteo ya ufaulu na kupelekea kuwa na upungufu wa vyumba hivyo 20. Kulingana na Mpango kazi wa Halmashauri vyumba hivi 20 vitakua vimekamilika ifikapo tarehe 15,Februari 2020
Mkurugenzi ameeleza kuwa mpaka sasa Ofisi yake imeshatoa shilingi milioni 260 kwa shule zote kuongezea nguvu kazi na michango mbalimbali inayotolewa na wananchi ambapo kwa sasa ujenzi upo katika hatua mbali mbali na kuleleza kuwa hakuna mwanafunzi hata mmoja atakayekosa masomo kutokana na uhaba wa madarasa.
Mkurugenzi huyo amezitaja shule hizo kuwa ni ;Alli Mchumo,Kibata, Nakiu na Kikanda zenye upungufu wa darasa moja moja, Pia alieleza kuwa shule zenye upungufu wa madarasa mawili kila moja ni; Kipatimu, Kiranjeranje,Kivinje, Mpunyule na Mingumbi huku shule ya sekondari ya Mtanga iliopo kata ya Masoko ikiwa na upungufu wa madarasa matatu.
Aidha Bwana Mchau ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wazazi wote kuwapeleka watoto wao kwenye shule walizochaguliwa bila kusubiri jambo lolote kwani maandilizi yote ya kuwapokea yamekamilika na hakuna kusubiri kwa kuwa maelekezo ya Serikali ni wanafunzi wote kuanza masomo mara moja kuanzia tarehe 06/01/2020 kama ilivyoelekezwa na Mhe. Waziri Mkuu. Aidha amewataka kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuchangia utekelezaji wa miradi hiyo ya ujenzi wa madarasa na miradi mingine ili kuharakisha maendeleo ya Kilwa na Taifa kwa ujumla
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa