kilwa,
Baraza la madiwani Halmashauri ya wilaya ya kilwa limeiomba serikali kubadili uamuzi wake wa kuchukua mapato yatokanayo na tozo ya Kodi ya Huduma kutoka katika kampuni iyanayo jihusisha na uchimbaji wa gesi katika kata ya songosongo.
Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika Mei 26 katika ukumbi wa Jumba la Maendeleo Mjini Kilwa Masoko, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Mhe. Abuu Mussa Mjaka amesema Halmashauri imesikitishwa na agizo la serikali la kutaka kuchukua mapato yanayotokana na Kodi ya huduma kutoka Halmashauri na kuyapeleka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Alisema iwapo maamuzi hayo yataanza kutekelezwa kwa vitendo, Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa itaathirika kwa kuwa pesa iliyokua ikipatikana kutokana na tozo ya Kodi ya Huduma ilikua inasaidia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Halmashauri.
“Tumelipokea kwa masikitiko makubwa sana agizo hili kwani lita tuathiri ndugu zangu, kwa sababu ile asilimia 0.03 ambayo tulikua tunaipata kama Kodi ya Huduma ambayo ni sawa na milioni mia sita mpaka mia saba kwa mwaka, Ilikua inatusadia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Halmashauri baada ya kutoa asilimia ishirini kwa ajili ya kijiji. Kwa maana hiyo kama hizo pesa zitaenda moja kwa moja Mamlaka ya mapato basi sisi tutakua tumepungukiwa na kiasi kikubwa katika bajeti zetu
Tuchukue fursa hii kuiomba serikali kusitisha mpango huu wa kuhamisha mapato yanayotokana Kodi ya Huduma kutoka Halmashauri kwenda Mamlaka ya mapato Tanzania ili wakazi wa sehemu ile ambayo gesi inapatikana na Halmashauri kwa ujumla iweze kufaidika na uwepo wa Gesi” alisema Mhe Abuu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya kilwa Mhe. Abuu Mussa Mjaka akihutubia katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika Mei 26 katika ukumbi wa Jumba la maendeleo Mjini Kilwa Masoko, kushoto ni makamu mwenyekiti Mhe. Swalehe Mohamed Mketo (Picha: Ally Ruambo)
Aidha Mhe. Mjaka amewatoa hofu wakulima wa zao la ufuta na wananchi wa kilwa kwa ujumla kuhusu mfumo utakaotumika katika uuzaji na ununuzi wa zao la ufuta msimu huu.
Mjaka amesema Halmashauri imejipanga kuhakikisha kuwa ufuta unauzwa kwa mfumo mzuri ambao utaleta tija kwa wakulima, Halmashauri na Taifa kwa ujumla.
“Mpaka sasa tumekwisha fanya vikao kadhaa kujadili ni mfumo gani ambao utatumika katika uuzaji na ununuaji wa ufuta msimu huu. Mifumo mingi ilipendekezwa ikiwemo wa stakabadhi ghalani lakini sisi kama Halmashauri tumechagua mfumo uliotangazwa na Waziri Mkuu wa kutumia minada kwa kua mifumo mingine tunaona inamkandamiza mkulima.
Tumekubaliana kuwa bei dira itakua ni shilingi 1764/= na leseni zote zitatolewa na Halmshauri ya wilaya ya kilwa na kwa wale watakoa hitaji kununua ufuta kutoka kilwa wanatakiwa kuwasilisha maombi yao ofisi ya Mkurugenzi mtendaji na watapatiwa utaratibu” alisisitiza Mjaka.
Mjaka amesema Halmashauri ya wilaya ya kilwa haijakubaliana na mapendekezo ya kukigawia Chama kikuu cha ushirika (Lindi Mwambao) shilingi 10/= kwa kilo kama gharama ya usimamizi na badala yake itatoa kiasi cha shilingi 2/= na shilingi 8/= itakayobaki itarudi kwa mkulima
“Mwaka huu tunatarajia kuvuna tani 15000 za ufuta kama mungu atajaalia, sasa unaweza ukapiga hesabu na kuona ni shilingi ngapi itaenda kwenye chama ikiwa tutakubali kuwapa hiyo shilingi 10/=, lakini tukifanya shilingi 2/= tutaokoa kiasi cha milioni 120/= ambazo zitarudi kwa mkulima ambae anatumia muda na gharama zake nyingi wake shambani” aliongeza mjaka
Pia amesema Halmashauri haijakubaliana na mapendekezo ya mkoa ya kukipa mamlaka ya kutoa leseni na kuitisha minada Chama kikuu cha ushirika (Lindi Mwambao) na kusisitiza kua shughuli zote kuhusu uuzaji wa ufuta zitafanywa na Halmsahuri yenyewe.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa