Katika kuimarisha huduma za usafiri na usafirishaji ndani ya Wilaya ya Kilwa, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Mohamed Nyundo, Tarehe 21 Julai 2025 amezindua rasmi Stendi Kuu ya Mabasi iliyopo katika eneo la Nangurukuru, Kata ya Kivinje Wilayani Kilwa, huku akiwataka wananchi kutumia fursa za kiuchumi zitazopatikana kupitia stendi hiyo.
Ujenzi wa stendi hiyo unatekelezwa kwa awamu ambapo katika mwaka wa fedha 2024/2025, Halmashauri ilitenga kiasi cha Shilingi 72,416,659/= kwa ajili ya kukamilisha hatua za awali, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya msingi inayowezesha stendi kuanza kutoa huduma kwa kiwango cha awali.
Pamoja na hatua hiyo, Halmashauri tayari imeanza mkakati wa kuendeleza stendi hiyo kuwa ya kisasa zaidi kwa kuwasilisha maombi maalum ya fedha Serikali Kuu.
Eneo la stendi lina ukubwa wa ekari 8, huku ekari 6 zikiwa tayari zimeendelezwa kwa matumizi ya awali ambapo Miongoni mwa kazi zilizotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa barabara za ndani, uwekaji wa taa za sola, ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua, pamoja na maandalizi ya maeneo ya maegesho ya vyombo vya usafirishaji vitakavyoingia katika stendi hiyo.
Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa tayari imekamilisha taratibu zote muhimu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) pamoja na Jeshi la Polisi na Usalama Barabarani, ili kuhakikisha kunakuwa na usalama kwa wananchi katika huduma za usafiri na usafirishaji.
Akiwasilisha Taarifa hiyo Ndg, Peter Ngoti, ameishuruku Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutoa dira na miongozo inayowezesha Halmashauri kutekeleza miradi yenye tija kwa wananchi.
Kwa upande wao wananchi waliohudhuria hafla hiyo wameonesha furaja yao kwa kupatikana stendi hiyo, huku wakiishukuru serikali kwa kuwaondolea adha ya upatikani wa eneo maalumu kwaajili ya upatikanaji wa huduma bora za usafiri na usafirishaji.
Mradi huu unatarajiwa kuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo kwa kuongeza fursa za ajira, biashara ndogondogo, na mapato ya ndani ya Halmashauri kupitia Sekta ya usafirishaji.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa