Kilwa,
Wajumbe wa bodi ya afya Halmashauri ya wilaya ya kilwa wametakiwa kuboresha huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma pamoja na kusimamia kikamilifu matumizi ya fedha kutoka serikalini na zinazokusanywa kutoka katika vyanzo mbalimbali.
Wito huo umetolewa na mkuu wa wilaya ya kilwa Mhe. Christopher Ngubiagai alipokua akizindu rasmi Bodi hiyo ofisini kwake Mjini Kilwa Masoko.
Ngubiagai amesema wananchi wanaimani kubwa na wajumbe hao na ndio mana wamewapatia nafasi ya kuwa wawakilishi wao katika bodi hiyo.
“Majukumu muliyopewa ni makubwa sana wananchi wamewaamini na mimi nawaamini pia, imani yangu hamutawaangusha katika utendaji wenu kwa muda wote mtakao kuwa wajumbe wa bodi hii” alisema ngubiagai
Ngubiagai amewataka wajumbe kutekeleza majukumu yao kwa kuutanguliza uzalendo mbele kwani kwa kufanya hivyo kutawasaidia kufikia malengo ya kuiinua Sekta ya afya Wilayani Kilwa.
“Uzalendo ndio nguzo muhimu itakayofanya tupate matokeo chanya. kama tujuavyo tuna changamoto nyingi sana katika hizi bodi zetu ikiwemo ya rasilimali fedha, sitarajii kusikia mmeshindwa kufanya vikao kisa mmekosa Fedha ya kulipana posho tunatakiwa kujitoa kwa moyo wote ikipatikana sawa ikikosekana sawa” alisistiza Ngubiagai
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Christopher Ngubiagai akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya Afya ya Wilaya ya Kilwa wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo (Picha:Ally Ruambo)
Pia amewataka wajumbe kuendeleza mema yaliyo achwa na wajumbe wa bodi iliyopita na kuongeza mengine ambayo yatakua yana tija kwa ustawi wa sekta ya afya.
Aidha Mhe. Ngubiagai ameahidi kutoa ushirikiano wa hali mali kwa wajumbe wa Bodi hiyo
“Hongereni sana kwa mara nyingine kwa kuwa wajumbe wa Bodi hii tusiogopane muda wowote kukiwa na jambo mnakaribishwa na nina ahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa mali na hali kama ambavyo tulikua tunashirikiana na kamati zilizopita” alihitimisha Ngubiagai
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya afya Wilaya ya Kilwa Bw. Adjuti Alli Adjuti amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa nasaha zake na kuahidi kuyafanyia kazi yale yote ambayo wameelekezwa kuyafanya na kusistiza ushirikiano miongoni mwa wajumbe.
Wajumbe wa Bodi ya Afya ya Wilaya ya Kilwa wakifuatilia mazungumzo ya Mkuu wa wilaya wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo (Picha:Ally Ruambo)
Awali akizungumza na wajumbe wa Bodi ya afya Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Mkurugenzi mtendaji wa Halmsahuri ya Wilaya ya Kilwa Ndg. Zablon Bugingo amewataka wajumbe kuwa mstari wa mbele kuwaeleza Wananchi ukweli juu ya uzushi ambao umekua ukizushwa na baadhi ya watu.
“Ndugu zangu tunawategemea sana kwenda kuwaeleza wananchi ukweli pale panapotokea uzushi kwa kuwa mnatoka moja kwa moja katika jamii inayotuzunguka itakuwa rahisi ukweli kufika, kumekua na fununu nyingi sana ambazo kimsingi hazina ukweli wowote kwahiyo ninyi wajumbe mtusaidie kuwaeleza ukweli wa mambo yalivyo’ alisema Bugingo
Aidha Bugingo amewataka wajumbe kuielekeza jamii juu ya utaratibu wa kuwasilisha malalamiko yao sehemu husika pindi wanapoona kuna jambo halijaenda sawa.
“Mtusaidie kuwaelimisha wananchi kuhusu suala la malalamiko, kuna watu wanakutana na changamoto mbalimbali wanapoenda kupata huduma lakini hawasemi wanakaa nayo na kusubiri aje kiongozi ndio wayaseme na wengine wanayafikisha ngazi za juu bila kuanzia chini, kwahiyo tukawaelekeze kuwa kuna hatua za kuwasilisha hayo malalamiko’ alisisitiza bugingo.
Mkurugenzi wa Halmashauri wa ya Wilaya ya Kilwa Ndg. Zablon Bugingo akizungumza na wajumbe wa Bodi ya Afya Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa (Hawapo pichani) kabla ya uzinduzi rasmi wa Bodi hiyo (Picha;Ally Ruambo)
Kabla ya kuzinduliwa kwa Bodi wajumbe walifanya uchaguzi na kumchagua Bw. Adjuti Alli Adjuti kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya afya Halmashauri ya wilaya ya Kilwa na Bi. Michaela Adeodatus Ngonyani kuwa Makamu mwenyekiti.
Kilwa Masoko
Anuani ya Posta: 160
Simu: 0672365354
Simu: 0672581557
Barua pepe: ded@kilwadc.go.tz /ictsupport@kilwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa